Wednesday, October 22, 2008

Wamachinga Dar kuanzisha benki yao

Wafanyabiashara ndogo ndogo al-maarufu kama `machinga`, wako mbioni kufungua benki yao itakayojulikana kama Tanzania Bank of Machinga Ltd, ambayo itawawezesha kuondokana na tatizo la kupata mikopo kwa ajili ya kutunisha mitaji yao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wauza Mitumba katika soko la Mchikichini, Bw. John Andrew, ameliambia Alasiri kuwa vikao kwa ajili ya maandalizi ya ufunguzi wa benki hiyo vimeanza.

Akasema benki hiyo imesajiliwa kwa Msajili wa Makampuni kama kampuni inayohitaji hisa na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni kuangalia jinsi ya kuhamasisha wadau wakubwa ambao ni wamachinga kununua hisa zitakazouzwa.


``Tumeshaanza maandalizi kwa ajili ya kuanza kuhamasisha ununuaji wa hisa. Jumamosi ijayo tutakutana vyama vyote ili kuweka mambo sawa,`` akasema Bw. Andrew wakati akizungumza na gazeti hili.

Akasema jumla ya hisa zenye thamani ya shilingi milioni 200 zitauzwa kwa bei ya shilingi 1,000 kwa kila hisa, lengo likiwa ni kuwawezesha wafanyabiashara wengi kumiliki hisa katika benki yao.

Akasema kwa mtaji wa shilingi milioni 150 tu benki hiyo inaweza kuanza na kwamba itaweza kukopesha watu ikifikia mtaji wa shilingi bilioni mbili.

Katibu huyo akasema kazi ya kukusanya fedha hizo ni rahisi kwa kuwa machinga wamehamasika kiasi cha kutosha baada ya kukumbana na masharti magumu wakati wanapotaka kukopa katika taasisi za kifedha.

Akasema masharti hayo yanatokana na taasisi za kifedha kutowaamini machinga katika suala zima la utoaji wa mikopo.

Akamshukuru Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Adam Kimbisa kwa kushirikiana nao katika suala zima la kuanzishwa kwa benki hiyo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo.

``Mheshimiwa Kimbisa ndiye aliyetoa wazo hili na amekuwa pamoja nasi kila wakati katika kutuwezesha kuanzisha benki hii, tunaomba na wadau wengine watusaidie,`` alisema Bw. Andrew.

`Akasema maandalizi hayo yamewashirikisha wajumbe kutoka katika vyama mbalimbali vya machinga ili kutoa hamasa kubwa ya ununuaji wa hisa.

SOURCE: Alasiri

No comments: