RAIS Jakaya Kikwete amezitaka benki nchini kufikiria zaidi namna ya kupunguza riba ambazo wakopaji katika benki hizo hutozwa warejeshapo mikopo.
Kwa kupunguza kiwango cha riba wanayotozwa wateja wa benki mbalimbali itasaidia kuwafanya watu wengi zaidi wakope pesa kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji.
Bw. Kikwete aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua rasmi Tawi la benki ya Stanbic mkoani Kilimanjaro.
Alisema kutoza riba kubwa ni mzigo kwa wakopaji na kwamba suala la riba kubwa limekuwa likichangia baadhi ya watu kutokopa kwenye benki.
Alitolea mfano kwa wawekezaji waombao mikopo kwa ajili ya miradi mikubwa ambayo huchukua muda mrefu kuanza kupata faida na kwamba biashara au miradi ya namna hiyo huhitaji riba ndogo.
"Kwanza nawapongeza kwa kukopesha wananchi wetu na hii ndivyo inavyotakiwa, kwani benki ambayo haikopeshi haina manufaa kwa nchi,” Aalisema Rais.
Kwa upande wa Serikali, alisema itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuangalia namna ya kuzifanya benki zisitoze wakopaji riba kubwa.
Awali Mkurugenzi wa Stanbic, Bw. Bashir Awale, alisema hadi sasa benki hiyo imekopesha kiasi cha sh. bilioni 31 katika sekta ya kilimo, sh. bilioni 30 kwenye sekta ya biashara, sh. bilioni 25 kwenye viwanda na sh. bilioni 49 kwenye sekta ya nishati.
Alisema benki hiyo ambayo ilikuwapo nchini tangu Machi 1911 wakati ikiitwa Standard British Bank of South Africa na ikiwa na tawi Zanzibar imekuwa ikiendesha shughuli zake kulingana na mabadiliko ya mahitaji ya wateja wake.
SOURCE: MAJIRA
Thursday, August 9, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment